
Ni maamuzi gani makuu matatu, ambayo ni muhimu kwa ubora wa maisha yako?
MAAMUZI ambayo yanasababisha wewe kuandaa mazingira
ya utajiri au umaskini katika muda wowote ule maishani mwako? Majibu ya
maswali haya sio siri na pengine sio mageni masikioni mwetu, ila
yanahitaji usikivu, ufuatiliaji, na umakini katika ufaniukishaji wake.
Hivyo basi, zingatia maamuzi haya makuu matatu yafuatayo, ili uweze
kubadili muelekeo wa maisha yako sasa hivi:
Uwamuzi # 1: Kuwa na Malengo Yanayoeleweka
Kuna ule usemi usemao “Mgaa gaa na upya hali wali mkavu!” Ndugu zangu
huu ni msemo mzuri kutoka kwa wahenga, lakini kama utakuwa unaamka
asubuhi kila siku na kuingia mtaani kwa mtindo wa “kugaa gaa”, basi jua
kwamba ni ngumu kufanikiwa, kwasababu hauna lengo linaloeleweka, yaani
kwa ufupi unabahatisha, na katika ubahatishaji kuna kupata na kukosa na
kama sio “mtu wa bahati” ndio hivyo tena Kwa mfano kama unataka kufanya
biashara, basi panga sasa hivi ni biashara gani unataka kufanya, na
fanya uchunguzi wa mambo yote yanayohitajika ili kuanza biashara hiyo.
Tafadhali tuwe wakweli katika hili, kwani tusije tukajidanganya
kwamba linalohitajika ni kufikiria tu biashara ya kuanzisha, la hasha!
Anzisha biashara, ambayo ipo ndani ya uwezo wako kwasasa na hakikisha
unaipenda hiyo biashara na isimamie kwa nguvu zote mpaka mwisho. Kama
mtaji wako ni laki 2 (zaidi au chini ya hapo), na hauna namna nyingine
yeyote ya kukuza mtaji huo, basi sio mwisho wa dunia, wewe anzia hapo
hapo ulipo kwa kufikiria nini kinaweza kikafanyika kwa mtaji huo ulio
nao. Mtaji mkubwa hauji kwa ndoto, anza kupanga mambo na kufanya sasa,
kwani wahenga walisema pia hata “Mbuyu ulianza kama mchicha.”
Kama wewe ni muajiriwa, basi fanya kazi kwa bidii sana, kiasi kwamba
huyo muajiri wako inafika mahala anaona biashara yake haiwezi kwenda
tena bila wewe kuwepo. Muda si mrefu utapandishwa cheo chenye malipo
zaidi au amini usiamini waajiri wengine wataona uchapaji kazi wako, na
watakuhitaji katika biashara zao kwa donge nono zaidi. Hivyo basi,
mwisho wa siku, uchapaji kazi unalipa iwe hapo ulipo sasa au sehemu
nyingine yeyote. Usiwe mtu wa kwenda kazini kwa lengo la kwenda tu, ili
mshahara wako uingie mwisho wa mwezi, unatakiwa uende kazini na
kuichukulia kazi yako kama mali yako binafsi na hapo ndio mafanikio
huanzia.
Uwamuzi # 2: Chukulia Changamoto za kimaisha Katika Mtazamo Chanya
Pindi unapopoteza kazi au biashara, pindi unapopata ajali, pindi
unapofiwa na mtu muhimu maishani mwako, au pindi unapopatwa na janga
lolote lile maishani, ni nini haswa unachofikiria? Je unafikiria huo
ndio mwisho wa maisha yako au mwanzo? Jinsi tunavyochukulia vitu (kwa
lugha sahihi) vinavyoitwa “changamoto” (sio “matatizo”) ni muhimu sana
kwani tofauti ya mitazamo ina athari kubwa sana katika mustakabali mzima
wa maisha yetu. Chukulia vitu hivyo vilivyotangulia kutajwa hapo juu
kama changamoto, ambazo zinakukomaza wewe kimaisha, hii ni pamoja na
kukosolewa na wengine.
Kama mtu anakukosoa katika kile ufanyacho, basi usione hatari, kwani
kukosolewa ni sehemu ya maisha na usione kila anayekukosoa ni adui yako.
Kuna mambo mengi sana ya kujifunza kutoka kwa wale tunaowaita “maadui”
zetu. Jifunze kufaidika na kunufaika kutoka kwa “maadui” zako, kwani kwa
kiasi kikubwa ndio watu pekee (marafiki na wapambe walio wengi hupenda
kutafuna maneno kwa kuhofia kukukera) ambao wapo tayari kutumia
mapungufu yako ya kibinaadam kukushambulia, na unaweza ukatumia fursa
hiyo kuimprove kwa faida yako.
Uwamuzi # 3: Jizuie Kufanya Maamuzi Yeyote ya Msingi Wakati Una Hasira
Wahenga pia walisema “hasira hasara!” Hivi umeshawahi kuzingatia
usemi huu kwa makini? Watu wengi hujikuta wakifanya maamuzi mazito
maishani mwao kipindi ambacho wana hasira kutokana na kwamba kama
binaadam hili ni rahisi sana kutokea. Lakini, sio lazima litokee kwako
pia kama utaanza kujizowesha sasa kuzuia kufanya maamuzi yeyote ya
msingi kipindi ambacho una hasira. Mke, mume, mteja, rafiki, na
kadhalika…wanaweza wakakupandisha hasira na utakuwa na kila haki na
sababu ya kukasirika, lakini hakikisha maamuzi yeyote unayotaka kuchukua
dhidi yao, yawe ni maamuzi ambayo umeyafanya kipindi ambacho hasira
zimetulia kama maji ya mtungi na mara nyingi huo ndio uwamuzi sahihi!
Tunataka kusikia maoni yako kuhusu dondoo hizi, wewe uzoefu wako katika maisha unasemaje?
Rungwe Jr.
0 COMMENTS:
Post a Comment