Kwanza, kabla sijaendelea embu tuwekane sawa kuhus hii falsafa ya
“kufanikiwa kimaisha”, ina maana gani haswa? Ukweli ni kwamba watu wengi
wakisikia fulani amefanikiwa kimaisha, basi moja kwa moja wanafikiri au
wanaamini mtu huyo atakuwa na pesa nyingiiii au kwa maneno mengine, mtu
huyo ni tajiri fulani hivi. Pamoja na kwamba pesa ndio mtatuzi wa
mahitaji mengi hapa duniani, lazima tukumbuke kwamba pesa ina uwezo wa
kununulia kitanda cha gharama kubwa sana, lakini ukashindwa kulala
katika kitanda hicho kwa msongo wa mawazo. Pia pesa inaweza ikakufanya
uopoe mwenza mzuri kuliko wote duniani, lakini mwenza huyo asiwe na
mapenzi ya dhati kwako.
Hapa tunajifunza kwamba ingawa pesa ni muhimu sana maishani,
kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mtu kimaisha hakuwezi kupimwa kwa kiasi
tu cha pesa alichonacho. Mtu anaweza akawa na pesa, lakini akakosa raha
kutokana na ukosefu wa amani ya ndani na nje ya mwili. Hivyo basi,
Kufanikiwa au kutofanikiwa maishani kwa mtu, ni lazima pia kupimwe kwa
mambo mengine muhimu kama uchamungu, ukarimu, maadili, busara,
uvumilivu, na ujasiri (wa kufanya na kuishi na maamuzi magumu). Hivi
“viambatanisho” 6 vya pesa ndio vinarutubisha na kudumisha pesa, na
zaidi humfanya mtu afurahie (enjoy) pesa hizo. Kwa uzoefu wangu,
mchanganyiko wa mambo haya yote muhimu, ndio humfanya mtu “afanikiwe
kimaisha” kwa maana pana ya falsafa hiyo. Baada ya muhtahsari huu,
tuendelee sasa na mada yetu, ambayo leo inagusia mambo makuu matano ya
watu waliofanikiwa kama ifutavyo:
#1: Huishi Kwa Siku Za Baadae (Future), Na Sio Siku Zilizopita (Past). Bila
shaka umeshasikia ule usemi wa siku nyingi kwamba “yaliyopita si
ndwele, tugange yajayo”. Watu waliofanikiwa kimaisha huwa na tabia ya
kutokatishwa tamaa na mambo ambayo yameshapita, na hayakwenda kama
walivyotarajia, kwani siku zote huwa wanakubali matokeo ya kutofanikiwa
kwao katika suala fulani na kujipanga upya kulikabili suala hilo. Siku
zote hujizuia kuruhusu matukio ya kushindwa kwao kufanikiwa katika
masuala fulani maishani, kushusha imani yao yakufanikiwa katika masuala
ya baadae (future).
#2: Hawalii Shida Na Wala Hawana Kinyongo. Hisia zako za
siku kwa kiasi kikubwa zinategemea na wapi ulipoelekeza mawazo yako. Kwa
mujibu wa mtaalam wa Saikolojia, Travis Bradberry, anaweka wazi kwamba “kama
umeelekeza mawazo yako kwenye shida ambazo zinakukabili, basi
unajijengea hisia hasi mwilini na kujiongezea mastresi kibao, ambayo
yana athiri na kuzuia uwezo wako wa kufanya mambo ya kimaendeleo”.
Hivyo basi, watu waliofanikiwa maishani huwa wanaelekeza mawazo yao
kwenye masuala chanya, ili kupiga vita mastresi na kujiongezea uwezo wa
kukomaa na mambo ya maendeleo. Pia, watu waliofanikiwa maishani huwa
hawaendekezi kinyongo, kwani wanaelewa kuwa kuweka kinyongo katika
masuala yaliyopita ni hatari sana kwa maendeleo. Vinyongo kama ilivyo
kubebea shida mbeleko, ni vitu ambavyo huzalisha hisia hasi mwilini na
kumfanya mtu kuwa na mastresi (au msongo wa mawazo), ambayo yana mzuia
kufanya mambo ya maendeleo.
#3: Hawatoi Kipaumbele Katika Ukamilifu. Hapa ina maanisha
kwamba, watu waliofanikiwa maishani huwa hawapotezi muda katika kutafuta
ukamilifu (perfection) katika mambo yao. Ni watu, ambao wanafaham
kwamba binaadam ni viumbe dhaifu na ukamilifu ni wa Mungu peke yake.
Hivyo basi, hii sifa inawasaidia sana linapokuja suala la kuridhika na
kile walichoweza kufanya baada ya kujitahidi kwa uwezo wao. Hii
inawafanya waendelee kujiamini, badala ya kujilaumu na kujihisi wamefeli
kama wale watu wanaolenga ukamilifu katika ufanyaji wa mambo yao.
#4: Hawapotezi Muda Wao Na Watu Wenye Mawazo Hasi. Hii sifa ni
muhimu sana na kwa ufupi ni muendelezo wa sifa #2, kwani ili mtu
aendelee kubaki na mawazo chanya kwa mustakbali mzima wa maendeleo yake,
ni lazima apinge kukaa na watu wenye mawazo hasi au walalamikaji. Kwa
ung’eng’e wanasema “ don’t hangout with negative people!” Hapa
wanazungumziwa marafiki, ndugu, na jamaa, yaani kuwa makini sana kuhusu
watu unaokaa na kuzungumza nao kwa siku. Kama watu hawa wamejaa
malalamiko tu kuhusu maisha yao siku nzima, basi jua wanagonjwa hatari
sana na ni watu wa kukaa nao mbali, ili wasikuambukize gonjwa hilo
hatari kwa maendeleo yako. Siku zote watu waliofanikiwa maishani (au
wale walio mbioni kufanikiwa) huwa wanajihusisha na watu wenye mawazo
chanya na matumaini tele kuhusu mustakbali wa maisha yao.
#5: Hawaoni Hatari Kusema “Hapana!” Hii pia ni sifa muhimu
sana, kwani watu wengi wanaostrago maishani, ni watu ambao wanataka
kumridhisha kila mtu, kitu ambacho ni kigumu sana. Mbali na kwamba sifa
moja wapo ya mtu aliyefanikiwa maishani ni ukarimu, watu hawa pia wana
ujasiri wa kusema hapana katika mambo ambayo hawataki au hawana muda wa
kufanya. Ni watu ambao hawazunguki mbuyu linapokuja suala la kumwambia
mtu kwamba ombi lao kwao limekataliwa. Hapa sio tu kwa wale watu
wanaopenda kupiga mizinga ya pesa (ambayo mengine haina msingi wowote),
bali pia kusema hapana linapokuja suala la kuombwa msaada wa kikazi na
washirika wa biashara au ajira. Watu waliofanikiwa maishani hawaoni
hatari kukataa kutoa msaada wa kikazi kwa watu wengine, ili kujipa muda
zaidi na uwezo wa kufanya kazi zao.
Anza kufanya uchunguzi wako leo kwa watu unaowafaham, ambao
“wamefanikiwa maishani” na utaona mifano hai ya sifa hizi au kama tayari
unawafaham watu hao, basi tupe maoni yako kwa faida ya wasomaji wote!
Rungwe Jr.
0 COMMENTS:
Post a Comment