
1.MALI ZIPI
HUTAKIWA HUGAWANYWA NDOA INAPOVUNJIKA? Ndoa inapotangazwa kuvunjika, mali
ambazo hupaswa kugawanywa ni mali za wanandoa wenyewe. Swali mbele yetu ni kuwa
ni zipi mali za wanandoa? Mali za wanandoa ni zile zote zilizochumwa na
wanandoa hao kwa jitihada au juhudi za pamoja wakati wa ndoa yao. Mali hizo
zaweza kuwa zinahamishika au hazihamishiki. Mali zisizohamishika ni kama
nyumba, viwanja, mashamba n.k. Mali zinazohamishika ni kama magari, baiskeli,
pikipiki,vifaa vya ndani kama fenicha, fedha benki, na mali nyingine ambazo
hazionekani kwa macho au hazigusiki kama hisa n.k. Zingatia sana usije
kudhulumiwa kwa kuwa hata hisa pamoja na akiba ya fedha benki nayo ni mali
inayostahili kugawanywa.
2. JE MALI ILIYOPATIKANA KABLA YA NDOA HUGAWANYWA?
Mali zilizopatikana kabla ya ndoa haziwezi kugawanywa ndoa inapovunjika
isipokuwa tu kama zilibadilishwa kuwa za wanandoa wakati wa ndoa. Swali ni
zinawezaje kubadilishwa kuwa za wanandoa? Zinabadilshwa kuwa za wanandoa iwapo
wanandoa walikubaliana kwa makubaliano maalum kuwa mali kadha wa kadha zitakuwa
zao wote. Na hii inaweza kuwa kwa maandishi au kwa kubadili majina ya nyaraka
za umiliki na kuzifanya kuwa na majina yote mawili ya wanandoa kutoka la mmoja
la awali.
Lakini pia zaweza kuwa za kwao wote kimatendo, kwa mfano kabla ya
ndoa mmoja wa wanandoa alikuwa na nyumba lakini haijamaliziwa. Wakati wa ndoa
nyumba hiyo ilimaliziwa kwa nguvu zao za pamoja na sasa imekamiliki. Nyumba ile
inageuka kuwa ya wote. Kwa ufupi maendelezo yoyote yanayofanywa na wanandoa
katika mali ambayo hapo awali kabla ya ndoa ilimilikiwa na mmoja peke yake,
yanaibadilisha mali ile kuwa ya ndoa. Hata kupaka rangi ni tendo la kuifanya
mali kumilikiwa kwa pamoja na hivyo kustahili mgao ndoa inapovunjika.
3. MAMA
WA NYUMBANI LAZIMA APATE MGAO NDOA INAPOVUNJIKA? Hapo juu wakati naeleza maana
ya neno mali za wanandoa ambazo hustahili mgao ndoa inapovunjika, nilieleza
kuwa mali hizo inabidi ziwe zimepatikana kwa nguvu, juhudi au jitihada au
mchango wa pamoja kipindi cha ndoa. Swali ni nini maana nguvu, jitihada, au
mchango wa pamoja? Watu wengi hujua kuwa juhudi au mchango wa pamoja
unaopelekea mali kuwa za wote na hivyo kustashili mgao ndoa inapovunjika ni ile
ya ‘leta nilete’. Yaani kama ni nyumba inajengwa mume akitoa saruji mwanamke
atoe nondo au mume akitoa hela na mwanamke atoe hela na kama ni gari mwanaume
akitoa milioni kadhaa na mwanamke naye achangie za kwake kadhaa na hapo ndipo
itakuwa mali yao wote na eti hapo ndipo mgao unapostahili. Hiyo ina maana
lakini finyu sana! Maana ya kisheria ya mchango au juhudi za pamoja hujumuisha
kazi anazofanya mama nyumbani wakati baba akiwa nje ya nyumba kwa uzalishaji
mali.
Kuosha vyombo, kupika, usafi wa nyumbani, kutunza na kuandaa watoto,
kufua, na kila kazi ya nyumbani ni mchango na juhudi ya pamoja kwa maana
niliyosema na lazima ilipwe kwa kugawana mali ndoa inapovunjika. Kwa maana hii
mama wa nyumbani hustahili mgao wa mali ndoa inapovunjika. Hii ni sheria na
kufanya hivyo ni lazima, si hiari wala hisani ya mtu.
4. KWA NINI SHERIA
IMEAMURU MGAO WA MALI KWA MAMA WA NYUMBANI? Sheria inamini kuwa wakati wa ndoa
mwanamke huwa ametoa sadaka maisha yake na utu wake katika kuwatunza watoto
(kama wapo) na kuitumikia familia kwa ujumla kwa kufanya kazi zote za nyumbani
kitu ambacho humwekea ugumu wa kuzalisha pesa na baadhi ya mali zitokanazo na
pesa. Sheria inaamini kuwa hilo hutokana na nafasi yake hiyo ya kuwa mwangalizi
wa nyumba wa muda wote. Hivyo basi haiwezi kuwa busara, hauwezi kuwa ubinadamu,
hauwezi kuwa utu, hauwezi kuwa ustaarabu, haiwezi kuingia katika akili ya
yeyote na haiwezi kamwe kuwa sawa kwa mwanamke kama huyo, baada ya talaka,
asipate chochote na aondoke bila chochote baada ya kuwa amepoteza miaka mingi
katika kuitumikia familia hiyo. Hii ndiyo sababu kuu ya kumpa mgao wa mali mama
ambaye hushinda nyumbani.
0 COMMENTS:
Post a Comment