February 10, 2013

FASTJET NDEGE ZENYE BEI NAFUU KULIKO ZOTE NCHINI HATARINI KUFUNGIWA.

Hi | 12:37:00 AM | |
ABIRIA wanaotumia ndege za shirika la ndege la Lonrho Aviation, maarufu kama Fastjet zenye bei nafuu kuliko ndege zote nchini, huenda wakakosa huduma hiyo kutokana na shirika hilo kuwa hatarini kufungiwa.

Shirika hilo huenda likafungiwa kuruka katika anga la Tanzania kutokana na kukiuka mkataba uliokuwapo kati yake na Fly540 Aviation Limited.

Sakata hilo limekuja baada ya kampuni ya Fly450 Aviation Limited kutangaza kuondoa leseni yake iliyotoa kwa Lonrho Aviation ili kuendesha shughuli za usafirishaji katika anga la Tanzania, Angola, Kenya na Ghana.


Kuondolewa kwa leseni hiyo kunamaanisha kuwa Fastjet sasa itapaswa kisheria kusimama kutumia alama au chapa zozote za Fly540 Aviation Limited, kampuni ambayo inasemekana iliuza hisa kwa mkataba ambao Fastjet wameukiuka.

Akizungumza kwa simu jana, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Fadhili Manonga, alithibitisha kupokea kwa barua toka kwa makampuni yote mawili yaliyowekeana pingamizi za kisheria.

“Ni kweli, tumepata nakala ya barua toka Fly540 Aviation Limited ikiitaka kampuni ya Fastjet kuacha kutumia alama au chapa zake kwa usafiri wa anga hapa nchini,” alisema.

Manongi aliongeza kwamba hawezi kuzungumzia kwa undani suala hilo kwani hiyo ni biashara yao ya ndani na kwamba kwa kuwa suala hilo ni mara ya kwanza kutokea kwa upande wao hapa Tanzania, kwa hatua za mwanzo aweza kusema bado wanasubiri ushauri wa wanasheria wao kuhusu mgogoro huo.

Alisema kuwa hilo suala linaweza kufika hadi mahakamani hivyo ni vigumu wao kwa hatua za mwanzo kulitolea tamko.

Timu ya waandishi wa Habari, ilifika katika ofisi za Fastjet kupata maelezo ya sakata hilo lakini watendaji wake hawakuwa tayari kutoa ushirikiano wa kutosha wakidai kuwa wasemaji wote wako ofisi zingine zilizoko Tazara.

Hata hivyo baada ya kubanwa zaidi, wasaidizi hao walidai kuwa wasemaji wakuu wa kampuni hiyo wako London na kuwa wanarekodi taarifa kisha sauti ya tangazo lao itarushwa humu nchini kupitia kituo kimoja cha redio.

0 COMMENTS:

Home of Technologies © Copyright 2010-2015 : Designed by : WebMaster