WAKATI wasanii wakubwa wa kimataifa wakiaminika kuwa kioo
cha jamii na mfano bora wa kuigwa na watu wengi, kitendo cha msanii Beyonce
Knoweles wa Marekani kukubali kuwa balozi wa kinywaji cha soda aina ya Pepsi,
kimelaaniwa na kukosolewa na wakereketwa wa masuala ya afya!.
Vyakula visivyo na
virutubisho (Junk Food) pamoja na vinywaji vyenye kiwango kingi cha sukari
ndivyo vinaaminika kuchangia kwa kiwango kikubwa ongezekao la magonjwa hatari
ya kisukari, shinikizo la damu na hata kiharusi, na siyo kwa watu wazima tu,
bali hata kwa watoto wadogo.
Kwa mujibu wa mwandishi mahiri wa masuala ya afya wa nchini
Marekani, Dk. Mercola, makampuni makubwa duniani ya vyakula visivyo na lishe
bora na makampuni ya vinywaji baridi, hutumia zaidi za dola za kimarekani
bilioni 2 (zaidi shilingi trioni 3) ku promoti bidhaa zao hatari ili zitumiwe
na watu wakiwemo watoto.
Ingawa jukumu la kuhakikisha mtoto anakula chakula na kunywa
vinywaji bora kwa afya ya binadamu ni la mzazi, lakini kitendo cha makampuni
hayo kutumia wasanii wakubwa kama Beyonce kwenye matangazo yao, kinaifanya kazi ya wazazi kutekeleza
jukumu lao kuwa ngumu.
Wengi tunapenda kuiga, hasa watoto, vitu vinavyofanywa na
watu maarufu, iwe kwenye chakula na hata muonekanao, hivyo staa kama Beyonce anapoonekana anatumia soda ya aina fulani,
si rahisi kumkataza mtoto kuitumia soda hiyo, hawezi kukuelewa!
Hivi karibuni, mwanamuziki huyo ameingia mkataba mnono wa
dola za Kimarekani milioni 50 (zaidi ya bilioni 80 za kibongo) ambazo atalipwa
na kampuni ya Pepsi kwa kuwa balozi wake wa dunia wa kinywaji hicho.
Wakati huku kwetu kitu chochote kinachopitishwa na wasanii
wa kimataifa kinaigwa kirahisi, hali ni tofauti kwa nchi kama
Marekani. Kitendo cha Beyonce kusaini mkataba huo kimezua mjadala mkubwa kuona
baadhi ya wanaojiita ‘mfano mzuri wa kuigwa’ (role models) hawafanyi kwa
vitendo vitu wanavyopaswa kufanya ili kuwa mfano mzuri wa kuigwa na jamii.
Kufuatia taarifa hizo za Beyonce, mtandao wa
frugivoremag.com umeandika maoni kadhaa ya kulaani kitendo hicho;
“Wakati baadhi ya
mashabiki wamefurahia mkataba wa Beyonce, wangine wamelaani kitendo cha kuunga
mkono kinywaji chenye sukari ambacho kinachangia matatizo ya kiafya ya
Wamarekani wengi hivi sasa.
“Wengine wamemtuhumu Beyonce kwa unafiki kwani upande mmoja
ameonekana kuungana na kampeni ya Baraka Obama na mkewe Michelle ya kuwahimiza
Wamarekani kujali afya bora za watoto, wakati upande mwingine anaunga mkono
kinywaji ambacho kinachangia matatizo mengi ya kiafya ya watoto wa Kimarekani.
“Wakati magonjwa hatari kama
Kutetemeka mwili (Parkinson’s Disease), magonjwa ya moyo, kiharusi na shinikizo
la damu yakiwa yameshamiri duniani, wengine wanalipwa mamilioni ya dola ili
kuimarisha magonjwa hayo,” aliandika pia mtoa maoni mmoja kwenye mtandao huo.
Utafiti uliyopo kuhusu unywaji wa vinywaji vyenye sukari
nyingi unaonesha kuwa matumizi yote ya vinywaji hivyo yana uhusiano mkubwa na
hatari ya mtu kuongezeka uzito wa mwili na kuwa tipwatipwa, hali ambayo
huongeza hatari ya kupatwa na magonjwa ya kisukari, shinikizo la juu la damu,
na magonjwa ya moyo.
Aidha, kila kinywaji cha ziada chenye sukari anachotumia
mtoto, huongeza uwezekano wa kuongezeka uzito na kuwa tipwatipwa kwa asilimia
60. Unywaji wa soda kila siku, unaongeza hatari kwa wanaume ya kupatwa na
ugonjwa wa moyo kwa asilimia 19. Unywaji wa vinywaji viwili au kimoja vyenye
sukari kwa siku, huongeza hatari ya mtu kupatwa na ugonjwa wa kisukari aina ya
pili, kwa asilimia 25!
Kimsingi, makapuni ya vinywaji baridi yanatumia mabilioni ya
pesa kila mwaka kutangaza biashara zao na kuzifanya zionekane hazina madhara
kwa watumiaji, hivyo hatuna budi kuelewa na kukubaliana na ukweli kwamba
avinywaji vyenye sukari, hata kama siyo pombe, ni hatari sana kwa afya zetu na
watoto wetu wako hatarini zaidi.
Tunashauriwa tusiwazoeshe watoto wetu unywaji wa soda na
vinywaji vingine vitamu na badala yake tuwazoeshe kunywa vinywaji halisi na
visivyo na sukari, kama vile juisi za matunda halisi bila kuweka sukari, maji
na vinywaji vingine kama hivyo. Kama huamini vinywaji baridi ni hatari, jiulize kwa nini
hivi sasa hata watoto wadogo wanaugua ugonjwa wa kisukari na saratani?
Tafakari, chukua hatua!
0 COMMENTS:
Post a Comment