
Safu
inayozungumzia kila kitu juu ya mapenzi. Ukiwa mdau wa kona hii, huwezi
kuwa mtumwa wa mapenzi na wala mapenzi hayawezi kukutesa. Utakutana na
changamoto za kawaida tu ambazo tayari utakuwa na silaha za kukabiliana
nazo.
Ni
kweli kwamba, kila binadamu ana haki ya kupenda, hili halipingiki hata
kidogo, lakini kulingana na mila na desturi zetu za Kiafrika wanaume
ndio huwa waanzilishi wa uhusiano.
Kwa
utamaduni huo basi, mwanamke hukosa uhuru wa kufikisha hisia zake kwa
yule aliye chaguo lake huku mwanaume akiwa huru kutoa dukuduku lake pale
anapohisi kupenda.
Pamoja
na kwamba maendeleo ya sayansi na teknolojia yanamfanya mwanamke wa
sasa awe na haki sawa na mwanaume, bado kumekuwa na ugumu kwa mwanamke
kumwambia mwanaume kuwa anampenda na angependa kuwa mpenzi wake.
Mwanamke
wa aina hiyo, huonekana mhuni, asiyejiheshimu. Lakini kuna jambo moja
la msingi hapa kulijadili; ni pale mwanamke anapotongozwa na mwanaume
asiye chaguo lake. Wakati mwingine inawezekana hata hajatongozwa, lakini
dalili za mwanaume huyo zikamfanya aone wazi kwamba anamtaka ila yeye
moyoni mwake akawa hana nafasi kabisa.
Hapa
ndipo wanawake wengi wanapobaki njia panda. Kwa bahati mbaya sana, wapo
ambao huamua kuingia kwenye uhusiano kwa majaribio, jambo ambalo ni
hatari kwenye uhusiano.
Inapotokea
hali hiyo baadhi ya wanawake wanashidwa kujua la kufanya na kufikiri
labda kuwajibu majibu ya hovyo huweza kufikisha hisia zao na kuachwa
kusumbuliwa.
Kama
yupo mwanaume anayekusumbua mara kadhaa na wakati mwingine kuona kuwa
ni kero kwako na hujui cha kufanya, usijali fungua ubongo ili uweze
kuongeza kitu kipya. Kuna baadhi ya wanawake wanafikia hatua ya
kuwatukana au kuwakejeli wanaume ambao wamekuwa wakiwasumbua kila
wakati.
Usijali,
kipo kitu cha kufanya. Zipo njia za kumweleza mwanaume husika humhitaji
kistaarabu na yeye asijisikie vibaya na ukamuacha akiwa mwenye
kukuheshimu siku zote za maisha yake.
NI MWANAMKE YUPI?
Kwanza
lazima nifafanue aina ya mwanamke ninayemzungumzia hapa. Kama upo
kwenye ndoa yako, vipengele vifuatavyo hapa chini havitakuhusu kabisa,
maana mwanaume anayemtongoza mke wa mtu, jibu lake ni mhuni.
Hana
staha na hafai kuthaminiwa na kupewa heshima ninayoizugumzia katika
mada hii. Kwanza, mke wa mtu ana alama. Zipo nyingi na zinajulikana hasa
kwa watu wanaomzunguka – wanamfahamu vizuri.
Ijulikane
kwamba hata huyo mwanaume anayekutongoza, anakufahamu vizuri; ikiwa ni
vinginevyo, huna sababu ya kujisumbua, huyo naye ni mhuni tu. Unajua
kuna baadhi ya wanaume, hawapitwi.
Kila
mwanamke anayemuona mbele yake, anamtaka. Hao siyo ninaowazungumzia
katika mada hii. Rafiki yangu, kama upo kwenye uchumba, una mwenzako
anayejulikana au hata kama hajulikani, jibu lako ni jepesi tu, una
mchumba!
Hutakuwa
na sababu ya kutumia njia hii. Njia hii ni kwa wanawake ambao wako huru
– wanasaka waume wa maisha yao, lakini kwa bahati mbaya, mwanaume
aliyekutamkia mapenzi, si cha chaguo lake.
Nimetoa
angalizo hilo kwa sababu, wanawake ambao tayari wako kwenye miliki za
watu, si busara kuruhusu mawasiliano au mikutano na watu wasio wao, tena
kuzungumzia mapenzi. Naamini nimeeleweka vyema. Sasa tuendelee...
MSIKILIZE
Hili
linawashinda wengi, lakini waswahili walisema kubali wito, kataa neno.
Kumsikiliza hakuna maana kuwa tayari umeshamkubalia. Kutana naye lakini
jitahidi kukwepa sehemu zenye vificho au ambazo utakuwa na wasiwasi
nazo. Kukubali kwako kutamfanya mwanaume huyu aone kuwa hujamdharau na
unamheshimu.
MPE UHURU AJIELEZE
Mwingine
anaweza kufaulu vizuri hatua ya kwanza ya kukubali wito, ila akifika tu
ataanza: “Sema haraka ulikuwa unasemaje?” au “Nina haraka bwana
zungumza haraka ulichoniitia,” na maneno mengine mengi yanayofanana na
hayo.
Hayo
siyo mambo, mwache azungumze, onyesha kujali mazungumzo yake na kuwa
makini kwa kila anachozungumza japokuwa tayari moyoni unatambua kuwa
haupo tayari kuwa naye.
Hakikisha
anafahamu kuwa mawazo yako yapo pale, hii itamfanya jamaa kuwa huru
kwako na kukueleza hisia zake kwa uwazi zaidi – si ajabu ukabadilisha
mawazo! Wiki ijayo tutaendelea na mada hii, USIKOSE!
Joseph
Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global
Publishers. Ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All
About Love vilivyopo mitaani.
0 COMMENTS:
Post a Comment